MTIZAMO WA IMAMU ALI JUU YA SERIKALI

Moja kati ya masuala yaliozungumziwa na kupewa kipau cha juu ndani ya kitabu kilichokusanya hutuba na hekima za Imam Ali (a.s) kijulikanacho kwa jina la Nahjul-Balagha, ni suala la serikali pamoja na uadilifu katika uongozi wa jamii.

Mtu yeyote atakayekisoma kitabu hicho mwanzo hadi mwisho, ataona jinsi Ali bin Abii Taalib (a.s) alivyolipa kipau mbele suala hilo, na kwa wale wafuasi wa dini zilizo nje ya Uislamu watakua ni wenye kushangaa sana na kujiuliza kua, hivi ni kwa nini kiongozi wa dini awe ni mwenye kushughulikia masuala ya serikali kiasi hichi, na atabaki kujiuliza, hivi kuna uhusiano gani kati ya masuala ya serikali na masuala ya dini?!

Lakini kwa wale wenye kuyatambua vyema mafunzo ya kidini  na kumtambua vizuri Ali (a.s), pamoja na kuelewa kua Ali (a.s) alilelewa na Mtume (s.aw.w) na kupata mafuzo yote yanayohitajika katika kuuongoza Uislamu tangu Yeye alivyokua mdogo hadi kufariki kwa Mtume (s.a.w.w),

Hawatolistaajabia suala hilo, bali iwapo Ali (a.s) hatolitilia mkazo suala hilo hapo ndipo wao watakua ni wenye kushangaa, kwani kiongozi kama Ali (a.s) hawezi kua ni mwenye kuyatupilia mbali masuala ya jamii, na moja kati ya masuala yanayohusiana na jamii, ni uongozi pamoja na uadilifu katika uongozi huo.

Kwani Qurani haikubainisha suala hili? Hebu iangalie Qurani inavyosema:

{Kwa hakika tumewatuma Mitume wazi wazi na tukawateremshia hukumu na tukawapa mezani (kanuni na sheria) ili wasimamishe uadilifu katika jamii}.

Katika Aya hii inaonekana wazi kua suala kutetea uadilifu ndio lengo kuu lililokusudiwa katika kutumwa mitume katika jamii tofauti za wanaadamu.

Vipi basi kiongozi kama Ali (a.s) awe ni mwenye kulipa kisogo suala hili?

Na ikiwa kuna watu wanaodhania kua dini imekuja kufafanua masuala ya sala tohara na mfano wa hayo tu, na kufikiria kua suala la uongozi liko upenuni mwa dini, watu hawa wanatakiwa kuzirudia akili zao na kufikiria kwa undani zaidi.

THAMANI YA SERIKALI NA UONGOZI KATIKA UISLAMU

 Suala la mwazo kabisa ambalo linatakia kueleweka, ni uzito na thamani ya suala la uongozi katika Uislamu.

Angalia Qurani inavyo muamrisha Mtume (a.s.w.w) kumteuwa Ali (a.s) kua ndiye kiongozi wa Waislamu baada yeke invyosema:

{Ewe mjumbe wa Mwenye Enzi Mungu fikisha ule ujumbe ulioamrishwa na Mola wako kuufikisha (kumteuwa kiongozi) na usipofanya hivyo utakua hukuufikisha ujumbe wake}.

Hivi kuna suala lililopewa umuhimu na kusisitizwa Mtume (s.a.w.w) kulifikisha kwa kupitia ibara kama ibara iliyotumika katika hii?

Katika matokeo yaliotokea katika vita vya Uhudi ilikua ni kuvipa mgongo vita na kukimbia huku makafiri wakiwanadia Waislamu kua Mtme (s.a.w.w) ameuwawa, hapo Qurani ikashuka na kusema:

{Muhammadi (s.a.w.w) si kiumbe wa aina yeyote, isipokua ni Mtume, kama walivyokua Mitume wengine waliotumwa kabla yake (huishi na kufariki),

hivi iwapo yeye atafariki au kuuwawa mtakua ni wenye kurudi nyuma na kuvikimbia vita?}   

Ustadh Tabaatabbi (mwandishi wa kitabu Almiizan fii tafsiiril Quran) katika makala inayozungumzia uongozi na serikali, ameifafanua Aya hii kwa kusema:

“kuuliwa kwa Mtume katika vita hakutakiwi kuwafanya watu waache vita na kurudi nyuma na kuwapa mwanya maadui, bali wanatakiwa wapiganaji hao kuendelea na mapambano na huku wakiwa chini ya kivuli cha yule aliyeteuliwa na Mtume katika uhai wake ili kuishika nafasi ya Mtume huyo endapo Mtume huyo atafariki au kuuwawa”.

Na kuna hadithi iliopokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) isemayo:

“endapo mkiwa safarini na idadi yenu ikawa ni watu watatu (au kendelea), basi mchagueni mmoja wenu awe ni kiongozi wenu”

Ukiitupia macho hadithi hii utafahamu kua, ni maumivu makubwa anayoyapata Mtume (s.a.w.w) pale anapoiona jamii ikikosa kiongozi huku ikisambaratia na kutokua na kiongozi wa kuitetea jamii hiyo.

Katika kitabu kilichokusanya hutuba pamoja hekima za Ali (a.s) kuna mengi yaliotajwa kuhusiana suala la serikali pamoja na uadilifu katika uongozi, nasi tutajaribu kuyazungumzia baadhi ya masuala hayo kadri iwezekanavyo.

Suala la mwazo linalotakiwa kuzungumzwa ni thamani na umuhimu wa serikali, Ali (a.s) kwa mara tofauti alitilia mkazo kuwepo kwa serikali imara iwezayo kuitawala jamii na kusimamisha uadilifu, huku akiwa ni mwenye kupambana na zile fikra za Makhawaarij (wafuasi wake waliomgeuka na kupingana nae) zenye madai ya kua Qurani ni yenye kutosheleza na wala hakuna haja ya kuwepo kiongozi maalum apasaye kutiiwa, na walidai kitabu cha Mwenye Enzi Mungu kinatosheleza, na sentensi hii wameitoa katika Qurani, kwani Qurani inasema kua hakuna mpangaji wa sheria isipokua Mwenye Enzi Mungu pekee, lakini Makhawarij waliitumia sentensi hii vibaya na kujaribu kuwazungusha watu akili zao, kwani madai yao yalikua ni kwamba hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kusimamisha serikali na utawala isipokua Mwenye Enzi Mungu peke yake.

 Naye Ali (a.s) anayajibu madai yao kwa kusema:

“nami ninasema kua hakuna mtu mwenye haki ya kusimamisha serikali na sheria isipokua Alla peke yake, lakini wenye kudai madai haya madai yao ni zaidi ya hayo, kwani wao wanadai kua Mwenye Enzi Mungu ndiye anayepaswa kua kiongozi hiyo serikali, hali ya kua jambo hili haliingii akilini, kwani Mwenye Enzi Mungu huiongoza jamii kwa kupitia waja wake, na jamii yeyote ni lazima iwe na kiongozi, ima kiongozi mwema au kiongozi muovo, kwani kua na kiongozi muovu ni bora zaidi kuliko kubakia watu kama wanyama, huku mwenye nguvu akimla aliye dhaifu, na jamii inapokua na kiongozi hapo ndipo watu wanapojihisi kua wapo katika usalama fulani wa kutenda kazi zao za kila siku, na hapo ndipo kila mtu hupevuka kwa upande wake, mwema hupevuka katika wema wake huku akiipalilia Akhera yake, na muovu hupevuka katika uovu wake huku akijivunia moto wake katika dunia hii ya starehe fupi.” Rejea kitabu

Nahjul-Balagha (äåÌ ÇáÈáÇÛå) hutuba ya arubaini.

  

Ali (a.s) hana tofauti yeyote ile na wacha Mugu pamoja na Mawalii wengine wa Mwenye Enzi Mungu katika kule kuliangalia kwake suala la uongozi (serikali) , kwani yeye haiangalii serikali au uongozi kua ni moja kati nyenzo zenye kuishibisha ile hisia ya njaa ya kujipatia umaarufu na ulua (madaraka), au kuichukulia kua ndiyo chanzo cha kuyafikia malengo ya maisha ya kudunia. Lakini iwapo serikali hiyo na uongozi huo utakua ni wenye kufuata misingi iliyo sawa, yaani ikawa ni yenye kusimamisha haki na uadilifu katika jamii, uongozi huu unahesabiwa kua ni moja kati ya amali zenye utakatifu wa hali ya juu kabisa mbele ya Ali (a.s), naye hua ni mwenye kuutetea uongozi huo kwa hali na mali ili usije kuangukia kwenye mikono ya wale wapenda madaraka wenye kutafuta mwanya wa kujipenyeza.

Siku moja Ibnu Abbas alimtembelea  Ali (a.s)  huku akia Ali (a.s) yuko  katika zama za utawala wake, akamkuta Ali (a.s) anavikarabati viatu vyake vilivyo kua vimechakaa,  Ali (a.s) akamuuliza Ibnu Abbas, hivi unafikiri viatu kua vina thamani yeyote ? Ibnu Abbas akamjibu, havina thamani yeyote, Ali (a.s) akamwambia, bila ya kusimamisha haki na uadilifu pamoja na kumpa kila mwenye haki haki yake, na kuondoa dhulma katika jamii, basi viatu hivi vitakua ni vyenye thamani zaidi kwangu mimi kuliko utawala nilionao mimi juu yenu. Rerjea kitabu Nahjul-Balagha (äåÌ ÇáÈáÇÛå) hutuba ya thalathini na tatu.

 

Na katika hutuba ya 207 amezungumzia kwa ujumla haki za wanaadamu baina yao na katika maelezo haya anasema:

Kila mmoja kati ya wanaadani ana haki maalum mbele ya mwenziwe, na moja kati ya haki zilizowekwa na Mwenye Enzi Mungu, ni haki zinazofungamana na wao kwa wao, na haki hizo amezifanya kua ni zenye kabiliana, kwa hiyo kila haki inayohusiana na mtu mmoja au inayohusiana na jamii haikamiliki bila ya kuwepo haki katika upande wa pili, kwa mfano iwapo mtu ana haki ya kukukopesha pesa basi ni haki yako wewe kumlipa pesa hizo, na haki hizi hua ni zenye kufungamana, kiasi ya kwamba kila mmoja anatakiwa kuitekeleza ile haki ilioko juu ya shingo yake hapo ndipo mambo yatapokwenda sawa katika jamii.

Ali (a.s) anaendelea kufafanua kua:

Na moja ya haki zilizomuhimu zinazowakabili wanaadamu, ni haki ya serikali juu ya wananchi na haki ya wananchi juu ya serikali yao na jambo hili ni wadhifa wa lazima juu ya wanaadamu wote duniani, na kuwepo kwa haki hizi baina ya wanaadamu, ndiyo rasililmali iwezayo kuwapatia mfumo utakaowanyayua na kuwapa heshima maalum katika jamii pamoja na dini yao. Wananchi hawatoweza kutengenea iwapo watakua wameteawaliwa na serikali isiyojali majukumu yake, na vile vile serikali katu haitotengenea iwapo watu watakua hawana msimamo na ukakamavu, basi iwapo serikali itayatekeleza majukumu ya ipaswavyo, na wananchi wakawa ni waaminifu na watiifu juu ya serikali yao, hapo ndipo haki itaposimama katika jamii na hapo ndipo jamii itapopata heshima yake, hapo ndipo misingi ya kidini itaposimama, na hapo ndipo alama na bendera za uadilifu zitapodhihi bila ya msokotano wa aina yeyote ile, na hapo ndipo kila kitu kitafuata njia yake ya kimaumbile bila ya kupinda na jamii hiyo itakua ni jamii madhubuti na yenye kupendeza katika zama zake, na maadui hawatokua na tamaa ya kuivamia jamii kama hiyo kwa kutokana na umadhubuti wake.  

THAMANI YA UADILIFU

Mafunzo ya dini ya Uislamu yameweza kuweka athari kubwa zenye thamani kwenye fikra za wanaadamu, mafunzo haya si tu yameweze kufungua milango mipya ya kielimu katika nyanja za kijografia na kibaiolojia pamoja na kijamii, bali mafunzo hayo yameubadilisha mfumo wa fikra za wanaadamu, na suala ni lenye umuhimu sana katika maisha ya mwanaadamu na jamii.

Ni bidii ya kila mwalimu kutoa mafuzo mapya yenye faida kwa wanafunzi wake, na kila mfumo unaokuja katika katika jamii hujaribu kutoa mafunzo mapya kwa ajili ya wafuasi wa mfumo huo, lakini ni mifumo michache inakuja na kuweza kuubadilisha mzima wa fikra za wafuasi wake na kuwafunza namna mpya kabisa ya kufikiri.

Mwanaadamu kwa kutokana na kua yeye ni kiumbe mwenye akili basi mawanaadamu huyu katika masuala yake yanayohusiana na  nyanja zote mbili, za kielimu pamoja na kijamii, hua ni mwenye kuzisimamishia dalili hoja zake, na katika dalili zake anazozisimamisha taka asitake hua ameitegemea misingi fulani katika kuzisimamisha dalili hizo. Na kwa kupitia misingi hiyo hiyo hua ni mwenye kukataa au kupitisha hukumu fulani. Na watu hutofautiana kifikra pale wanapokua ni wenye kutofautiana katika misingi hiyo, misingi ambayo hutumika pale mtu anapotaka kusimamisha dalili zake au kullihukumu suala fulani, kwa natija na jawabu ya kila katika fikra zake hutegea ni misigani aliyoitegemea mtu huyo katika kufikiri kwake, hili ndilo linalosababisha watu kutofautiana kifikra.

Kwa kawaida katika katika masuala ya kielimu, hua hakutokei tafauti za kifikra baina ya wataalamu wa elimu Fulani wanoishi zama moja, na ikiwa kuna tafauti fulani inayoonekana baina ya baina ya wataalamu wa elimu fulani, basi tofauti hiyo itakua imesababishwa na kutoka na kua wataalamu hao hawakua wakiishi katika zama moja. Lakini katika masuala ya kijamii utakutia kua watu wanaishi katika jamii moja na zama moja, lakini watu hao wanatafautiana kimaumbile, kitabia, kivazi, namna ya uchanaji wao wa nywele, ubabe, uchokozi, n.k, na suala hili kwa kweli hatuna nafasi ya kulizungumzia hapa.

Pale mwanaadamu anapokabiliana na tabia pamoja na masuala tofauti ndani ya jamii fulani, taka asitake atakua ni mwenye kutoa hukumu fulani nje au ndani ya akili yake juu ya jamii hiyo, na kila moja kati ya yale aliyokumbana nayo katika jamii hiyo atakua amelipa thamani hukumu maalum kwenye akili yake, pengine moja litakua ni zuri kwa mtizamo wake na jengine liwe baya, basi lililo baya kwa laweza kua ni zuri kwa mwengine, hii inatokana na watu kutofautiana katika ile misingi yao mikuu ya kufikiri.

Kwa mfano suala la kujihifadhi kwa mwanamke pale anapokua katika jamii, bila shaka watu wametofautiana katika suala hili, kuna wale wanaoona kua suala hili ni la lazima mwanamke, ma kuna wengine wanaodai kua suala hili halina umuhimu wowote katika kuijenga jamii.

Basi pale tunaposema kua Uislamu umeleta mapinduzi katika fikra za wanaadamu, tunakusudia kua Uislamu ulipokuja uliyakuta baadhi ya mambo yaliyokua hayapewi thamani ndani ya jamii ukayapa thamani, na kuna mengine yaliyoonekana kua ni yenye thamani ukayashusha thamani, moja kati ya yale yaliyopewa thamani na Uislamu ni Ucha Mungu, Uislamu ulipokuja ulilitilia mkazo suala hili na kulipa thamani ya hali ya juu kabisa, na Mwenye Enzi Mungu akaahidi zawadi yenye thamani kubwa kwa kila atakayelitilia mkazo na kushikamana na suala hilo, na moja ya yale yaliyoshushwa thamani na Uislamu ni ukabila, suala ukabila lilikua ni lenye kupewa kipau mbele sana kabla ya kuja kwa Uislamu, lakini Uislamu ulipokuja ulilishusha daraja suala hili hadi thamani ya suala hili ikagonga zero katika kushuka kwake thamani.   

Uadilifu ni suala ambalo limepewa uhai na uzito mkubwa pale  Uislamu ulipodhihiri, hebu basi tuzibue masikio yetu na tumsikilize Ali (a.s) jinsi anavyolifafanua suala hili:

Mmoja kati ya watu washupavu waliokua katika zama zake alimkabili Ali (a.s) na kumuuliza:

“kipi bora kati ya uadilifu na usamehevu?” Ali (a.s) akajibu kua

uadilifu ni bora kuliko usamehevu akifafanua kua uadilifu ni maana yake ni kukiweka kila kitu katika sehemu yake inayostahiki kuwekwa lakini usamehevu ni kuto kuweka kitu katika sehemu yake. Kwakuchangia suala ili ilieleweke tunaweza kusema kua:

1-    hii ni kwa sababu uadilifu una maana ya kua kila alipwe kwa kutokana na thamani ya kazi yake, lakini usamehevu haumaanishi hivyo bali hua ni kuto kumlipa mtu kwa lile alilolitenda miongoni mwa maovu yake.

2-    Uadilifu ni msingi mkuu wa kanuni na ndio bakora imara ya iwezayo kuichunga jamii kwa ukamilifu, na ndio bara bara kuu ya jamii, kiasi ya kwamba hakuna jamii iwezayo kutembea nje ya bara bara hiyo bila ya kukutwa na maafa, lakini usamehevu ni moja kati ya masuala ya dharura kwa sababu asili hasa ya mtenda uovu ni kuadhibiwa, lakini kwa kutokana na dharura fulani mtu huyo hua ni mwenye kusamehewa.

Kwa hiyo kati ya uadilifu na usamehevu uadilifu ndio unaochukua nafasi ya kwanza. Rejea Nahjul-Balagha hekima ya 429.

Mbele ya Ali (a.s) uadilifu ndio uwezao kuiweka sawa mezani ya jamii pamoja na kuiweka salama na kuituliza jamii hiyo, na dhulma haiwezi kuisaidia jamii chochote kile na hata mfanya dhula si mwenye kupata utulivu kwa dhulma yake, na siku zote roho yake hua juu juu tu, lakini uadilifu ndio njia kuu inayoweza kuikubatia jamii nzima na jamii hiyo hatopata mgongano wa aina yeyote ile katika kutembea na kuendelea na msafara wake katika njia kuu hiyo, dhulma njia isio na macho isioweza kumuongoza yeyote ile, hata mfanya dhulma mwenyewe haiamini njia hiyo, kwani wakati wowote ule yaweza kumtupa njiani bila ya kumfikisha mwisho wa safari yake.

Sisi sote tunaelewa jinsi Othman alivyofanya katika ukhalifa wake na hasa pale alipokua akizigawa pesa za benki ya waislamu (Baitul mali) na kuwapa watu karibu yake, basi zizipofikia zama za utawala wa Ali (a.s) watu walikua wakimwabia Ali (a.s) kua yeye asiafuatilie mambo yaliokwisha pita bali ashuulikie tu yale yanayotokea katika zama zake na awachane mbali na kufuatilia haki zilizopotezwa na Othman, Naye akawajibu kua, haki itabakia kua ni haki hata kama itakua imepitiwa na muda na kukonga, na ni lazima kufuatiliwa bila ya kupuuzwa. Na alivyokua akijibizana na watu hao aliwaambia hivi:

Naapa kwa Mola wangu kua iwapo kutakua kuna mtu aliyechukua mali kaitka zama za Othman kinyume na sheria, basi mali hizo nitazirudisha mahala pake, hata kama atakua ameziolea au kuzinunulia mjakazi pia sitomuachia.

Kwa hakika uadilifu ni mlango mpana, basi ikiwa kuna mtu anayehisi kudhikiwa kubanwa na mlango huo basin a aelewe kua dhulma ni yenye kudhiki na kubana zaidi. Reja Nahjul-balagha hutuba ya 15.

Ali (a.s) anauhesabu uadilifu kua ni wadhifa wa kidini wa kila mtu, bali ni moja kati ya mipaka ya mwenye Enzi Mungu isiopaswa kukiukwa, na Ali (a.s) hakua ni mwenye kuridhika kumuona Muislamu asiye tofautisha baina ya haki na dhulma katika jamii.

 Ndani ya kitabu cha Nahjul-balagha mna hutuba iitwayo Shaqshaqiyya, ndani ya hutuba hii utakuta namna gani Ali (a.s) anavyoelezea masikitiko yake kutokana na ubovu wa siasa uliotokea katika serikali zilizopita, zama ambazo watu walikuwa wamechoshwa na matatizo ya siasa hizo, kiasi ya kwamba baada tu ya kuuliwa Othaman, watu walimsumbua Ali (a.s) kila wakati na kumtaka ashike madaraka, huku Ali (a.s) akijaribu kuyakimbia madaraka hayo yaliyo na majukumu mazito ndani yake, hasa hasa kwa kutokana na uharibifu uliokua umefanya na viongozi waliopita kabla yake, pamoja na fitina na khiana alizofanyiwa Yeye mwenyewe na watu wa jamii yake, hayo yote yalimfanye Yeye asiwe na hamu tena ya kushika uongozi. Lakini kwa kutokana na kufhofia kua iwapo Yeye hatoshika madaraka watu wa jamii yake watazidi kuteketea, huku baadhi yao wakilia njaa na wengine wakilia kutokana na dhulma pamoja na kukhofia jamii kutogawika sehemu mbili huku sehemu moja yenye madaraka kuwakandamiza wasio na madaraka, hayo kwa ujumla ndio yaliomfanya Ali (a.s) kukubali kushika madaraka hayo.

Na hapo Ali (a.s) alisema:

“ingelikua si lile kundi la watu lililonishindikiza kushika madaraka, na ingalikua si  wajibu juu yangu kulibeba jukumu hili, nisingekubali kuchukua jukumu hili. Lakini ni lazima juu ya wanazuoni na wenye elimu kuto nyamaza pindi waionapo dhulma itendapwo, na ingalikua sio hivyo, basi ningelikaa kando kama nilivyokaa kando katika zama za makhalifa waliopita.

UADILIFU HAUTAKIWI KUWEKWA KANDO KWA SABABU YA MANUFAA FULANI

Hivi leo ubaguzi, kuteuana na kupeana kazi kijamaa, kubwagia tonge kubwa kubwa za rushwa, ndio mambo yalioenea idarani mwote, na mambo hayo yamegeuzwa kua ni moja yati ya nyenzo za kisiasa na kuendesha nchi katika jamii, lakini unahodha wa jahazi ya kisiasa ulipomfikia Ali (a.s) hayanyamazia mambo hayo na badala yake Yeye alikua ni adui wa mambo kama hayo, lengo lake lilikua ni kupiga vita siasa za aina kama hiyo, hilo ndilo lililowafanya wanyonyaji walioko serekalini kukasirika na kuto ridhika na uongozi wake, na hicho ndicho kikawa chanzo cha fitina katika utawala wake, hapo ndipo baadhi ya marafiki wa Ali (a.s) walipomwendea na kujaribu kumpa mawazo na kumwambia: “kwa kutokana na maslahi yako na usalama wako, basi waonaje  kama utaachilia mbali suala la kuweka haki sawa katika jamii, hasa hasa ukizingatia kua wenye kulipinga suala hili ni miongoni mwa Masahaba ambao ni maaadui wako, huku ukizingatia kua baadhi ya maadui hao wameshika madaraka ktika sehemu zilizo muhimu, kama vile Muaawiya aliyeshika madaraka katika mji wa Shaam.

Basi jiepushe na matatizo kwa kutoyaingilia masuala yao na dhulma wanazozifanya”.

 Ali (a.s) aliwajibu kwa kusema:

“hivi mnanitaka nijitafutie ushindi na madaraka kwa kupitia dhulma? Mnanitaka mimi niuchinje uadilifu kwa kupitia kisu cha siasa? Naapa kwa kwa Mwenye Enzi Mungu kua, mimi sitoyafuata mawazo yenu, bali nitashikamana na uadilifu, na hata kama ingalikua mali hii iliokuwepo katika benki ya Waislamu ni mali yangu binafsi, basi nisingelibagua katika ugaeaji wa mali hiyo katika jamii bali ningaliigawa mali hiyo kwa usawa, basi vipi mimi leo nifanye ubaguzi katika mali ya Mwenye Enzi Mungu iliowekwa amana kwangu name si mmiliki wa mali hiyo.

Hivi ndivyo Ali (a.s) anavyo yafanyia tathmini anayopewa kabla ya kuyafanyia kazi na hivi ndivyo Yeye anavyoitathmini jamii.

HAKI ZA WATU KATIKA JAMII

Wanaadamu wana mahitajio tofauti kama vile chakula, kivazi pamoja na makazi, ni rahisi kuweza kumtekelezea mnyama kama vile farasi au njiwa mahitajio yake, hii ni kutokana kua yeye hana makuu bali anaitajia kula na kunywa pamoja na usalama wa mwili wake, lakini kumtekelezea manaadamu mahitajio yake si jambo lililorahisi, kwani mwanaadamu ana mahitajio ya kimwili pamoja na mahitajio ya kiroho yawezayo kuituliza akili yake.

Si jambo gumu sana kwa serikali kuweza kuitimizia jamii mahitajio ya kimwili kwa usawa bila ya kubagua, lakini ni vigumu serikali hiyo kuweza kuyatekeleza mahitajio ya jamii ya kiroho, hii ni kwa kutokana na kua kila mmoja ana maradhi maalum yanayoisumbua roho yake na mara nyingi maradhi hayo hutofautiana kwa jinsi ya watu walivo.

Moja kati ya mambo yenye kuifanya jamii iridhike na serikali yao ni mtizamo wa serikali juu ya jamii hiyo, na vipi srikali hiyo inavyojiangalia pamoja na kuiangalia jamii hiyo, je serikali hiyo mtawala ma ndiye bwana wa jamii? Au ni wakili alieteuliwa na jamii hiyo kuyatekelea matakwa na mahitajio ya jamii? Katika sura ya kwanza serikali hua ni kama raisi wa jela ya wendawazimu au mchunga punda ambaye hujihisi kua yeye ndiye mmiliki halisi wa punda hao na ana haki juu ya punda hao, basi huwalisha punda hao atakavyo na kuwaongoza atakavyo. Na ikiwa serikali itakua ni wakili aliye chaguliwa na jamii yake ili kuyatekeleza matakwa ya jamii hiyo, basi serikali hiyo itakua ni mhudumu aliye muaminifu wa jamii hiyo. Kukubali kwa serikali kua jamii ilioichagua serikali hiyo kua ni yenye haki maalum na kuto kutenda amtendo yenye kuonyesha kuwepo kwa ukiukaji wa haki za jamii, ni moja kati vivutio vitakavyoifanya jamii hiyo kua na matumaini pamoja na kuiridhia serikali yao.

Sote tunaelewa kua katika karne zilizopita Ukiristo ulikua umshika hatamu katika nyanja tofauti za kidini na kidunia, lakini kwa kutokana na matendo ya Kanisa yalivyokua si yenye kuziridhisha nyoyo za watu pamoja na kushindwa kwa Kanisa katika kuyatimiza mahitajio ya jamii, jambo ambalo limesababisha jamii ya kimagharibi kuhisi kua dini haina uwezo wa kuyatimiza mahitajio ya wanaadamu, na linaloonekana hivi sasa katika jamii ni kuikimbia dini na kuivamia dunia kwa kutapatapa huku wakidhani kua matamanio yao ndiyo yawezayo kuiongoza nafsi ya mwanaadamu.  

Baada ya viongozi wa Kanisa kutoa hukumu na mitizamo kwa kupitia rai zao bila ya kua na elimu yakutosha, na kujihisabu kua wao ni wateuliwa wa Mwenye Enzi Mungu huku matendo na fikra zao zikienda kinyume na hali halisi ya kilimwengu, jambo hili liliwafanya watu kutoridhika nao, hasa hasa pale walipokua wakipingana vikali na mitizamo ya kielimu na kifalsafa iliokua ikitolewa na wanazuoni walioko katika zama zao.

Hapo ndipo watu walipohisia kua ima wamkubali Mungu na kukubaliana na serikali inayodaiwa kuwa ni serikali ilioteuliwa na Mugu, serikali ambayo viongozi wake hawakua na ubora wa aina yeyote juu ya watu wengine na hawakua na tofauti na watu wengine wa jamii hiyo, au wamkatae Mungu ili wawe huru na kuepukana na serikali yenye kuwakandamiza watu kifikra na kielimu.

Katika mtizmo wa kisaikolojia ya kidini, ni kua moja kati ya mambo yenye kuirudisha dini nyuma ni kuwepo mgongano baina ya fikra zinazotangazwa  na dini hiyo katika jamii na fikra za watu wanaoishi ndani ya jamii hiyo, hasa hasa iwapo fikra hizo zitakua zimeenea katika jamii nzima. Tatizo hili kwa upande wanchi za kimagharibi lilitokea wakati ambapo jamii ilikua na kiu ya kelimu, kawa upande mmoja jamii ilikua ikihitajia kujitawala wenyewe na kuithibitisha misingi yao ya kielimu, na kwa upande mwengine Kanisa halikuridhika kuipa jamii uhuru huo, kwani Kanisa lilikua na mtizamo wa kua jamii haina mamlaka yeyote katika utawala, bali inatakiwa kusikiliza na kuitii serikali bila ya kuhoji chochote, na hii ilikua ni sababu tosha ya kuifanya jamii iichukie dini na kuanza kupingana na yule Mungu aliyedaiwa na serikali hiyo huku wakiwa na hisia ya kua Mungu na dini iliyoletwa na Mungu huyo ndivyo vinavyowakandamiza na kuwanyima uhuru wa kufikiri na kuzitangaza fikra zao za kielimu.

Suala la ukandamizaji wa jamii halikuanza leo bali mizizi yake ilikuwepo tangu zama za kale.

Mwana falsafa maarufu ajulikanaye kwa jina la (filon) ananukuu kutoka kwa kiongozi wa Roma ya zamani aliyekua akisema kua “hakuna tofauti baina ya mchunga kondoo na kiongozi wa nchi, kwani mchunga kondoo ni mtukufu na mbora juu ya kondoo anaowachunga, na kiongozi wanchi vile vile ni mbora na mtukufu kuliko raia wanchi hiyo, kwa hiyo viongozi ni kama Miungu katika jamii na jamii ni kama wanyama wenye kumilikiwa na Miungu hiyo”.

Vile vile Mr Gorsius ambae na mwandishi watarehe mwenye asili ya ki Holand alieandika kitabu kijulikanacho kwa jina la (Haki vita na amani) anasema kua viongozi  si kwa ajili ya kuwahudumia raia bali raia ndio wanaotakiwa kuwahudumia viongozi wao, na anaitolea dalili kauli yake akisema: “kama ilivyokua watumwa wanawatumikia mabwana zao hivyo ndiyo ilivyo jamii mbele ya viongozi wao.

Na Mr Habz (mwana philosophy) nae ana mtizamo kama huo, kwa mtizamo wa wanafalsafa hawa ni kua watu ni kama makundi ya mbuzi au kondoo, kila kundi moja lina kiongozi wake maalum analolishughulikia na kulichunga kundi hilo.

Mr Roso (mwana philosophy) haki hii ya uongozi anaiita kua ni haki ya uongozi wa mabavu na akilizungumzia suala hili anasema:

“nguvu zote zinatokana na Mungu na watu wote wote wenye nguvu yeye ndiye aliyewaleta, lakini hii haimaaanishi kua sisi tusifanye jitihada za kuwaondoa watu hao wenye nguvu madarakani, kwani magonjwa yote yameletwa na Mungu lakini hilo haliwafanyi watu wajizuwie kwenda kwa dokta na kutaka matibabu, hivi iwapo mwizi atanivamia hivi mimi ninatakiwa kusalimu amri kwa kua yeye ana nguvu au natakiwa nijitahidi kupambana na mwizi huyo, basi ikiwa mimi ninasilaha ya kupambana na mwizi huyo lakini kwa sababu yeye ana nguvu nkasalimu amri, basi kuna maana gani ya kuwepo kwa silaha?

Mr Habz katika mtizamo anaonekana kua katika suala dhulma za viongozi, hakubaliani na fikra za kudai kua viongozi wa haki ya kutenda walitakalo katika jamii bila ya kuingiliwa na mtu yeyote, na katika mtizamo wake wa kifalsafa unaozungumzia haki za kisiasa ni kua viongozi ni watekelezaji wa matakwa ya jamii na niwenye kuonyesha sura halisi ya jamii, na lolote lile lifanywalo na viongozi hao hua ni lenye kutoa sura kamili ya fikra na matakwa ya jamii ya viongozi hao, lakini tukimpekua zaidi Mr Habz

 tutakuta kua yeye ameathiriwa na fikra za Kanisa kwani yeye anadai kua utawala wa mbavu haupingani na uhuru wa wanaadamu angalilia kauli zake zisemavyo:

haitakiwi kudhania kua kuwepo kwa uhuru katika jamii kunatoweka kwa kuwepo uongozi uongozi wa kimabavu, kwani tunaelewa kua chochote kile kinachotendwa na viongozi hua ni kama kua kimetendwa na jamii, kwani serikali hua ni yenye kutoa picha ya matakwa ya jamii katika matendo iyatendayo serikali hiyo

kwa hiyo tendo lolote lile litendwalo na serikali haliwezi kutwa dhulma, kwani tendo hilo hua ni kama kwamba limetendwa na jamii yenyewe. Basi hata kutakuwepo kiongozi atakaesbabisha baadhi ya watu kuuwawa haitakiwi kiongozi huyo kuitwa dhalimu, na watu wote wanatakiwa kuzitii amri zilizopangwa bila kubagua hukumu hizo kwani watu ni waja wa Mungu na Mungu ndiye aliyetaka wazitii serikali zao Naye ndiye aliyewapa serikali hizo. Yaweza kutokea kiongozi atakayesababisha kifo cha mtu fulani, lakini hilo halihesabiwi kua ni kosa, bali kitendo hicho tuaweza kukifananisha na kitendo cha Yaftaa ambaye alikua ni mmoja kati ya viongozi (Kadhi) wa Kiisraaili aliyeweka nadhiri kua iwapo tashinda katika vita alivyokua akipigana, basi mtu wa kwanza atakayekutana wakati atakaporudi kutoka vitani atamchoma moto na kumtoa muhanga kwaajili Mwenye Enzi Mungu, na alipokua akirudi mtu wa mwanzo aliyekutana naye alikua ni binti yake, hapo basi alimkamata na kutekeleza nadhiri yake. Basi mtu hua yuko huru katika kulitenda lile lenye kumsababishia kifo au kutolitenda tendo hilo, na hata kama kiongozi atauwa watu bila ya hatia, atakua hakumdhulumu mtu bali amemdhukumu Mugu kama vile alivyofanya Daudi pale alipomuuwa Uriyaa (Jaaluut).

Rejea kitabu (Qaradaade ijtimaai) kilichoandikwa kwa lugha ya Kipashia (Kifarsi).