NGUZO NNE ZA IMANI

Imani imesimama kwenye nguzo nne: Uvumilivu, Uhakika, Uadilifu na Jitihada (Imam Ali (a.s.) – kitabu cha Nahjul Balagha)

Endapo tunafikiria meza yenye miguu minne, na mojawapo wa miguu hiyo unaondolewa, je! Meza bado itakuwa na nguvu ile ile? Ikiwa na miguu mitatu tu itatingishika sana; hivyo kwamba ikitikiswa kidogo tu itaanguka na kila kitu kilichomo juu yake kitaanguka chini. Au tunaweza kudhani nyumba ambayo inasimama juu ya nguzo nne. Kama nguzo moja ikiharibiwa zingine tatu hazitaweza kuhimili uzito wake na itaporomoka na kuwaangukia wakazi wake. Imam Ali (a.s.) ameieleza imani ya muumini kwa njia ile ile, na ameorodhesha masharti makuu manne yanayo himili imani. Endapo mojawapo ya hayo ni dhaifu imani ya muumini haitakuwa kamili, na kama haikurekebishwa, muumini anaweza kupoteza nguzo ya imani na kuhatarisha imani yake.

Kwa ufupi tutazungumzia haya masharti manne, na katika yote hayo, uvumilivu ni muhimu sana, kwa hiyo tutalizungumzia mwishoni..

1.              Nguzo ya pili – Uhakika

Uhakika maana yake ni kwamba mtu haamini tu kitu hivi hivi isipokuwa pawepo na imani kamili kwamba kitu kile ni cha kweli. Zipo hatua tofauti kwenye imani ambazo mtu anaweza kuwa nazo. Mtu anaweza kuamini kitu kwa msingi wa akili na mantiki, na hii ni hatua ya kwanza. Mathalani, tunapoona mawingu ya mvua yanakuja kwenye anga ya mbali, tunaamini kwamba leo mvua itanyesha. Mawingu ni ishara ya kuja kwa mvua. Au kama ardhi ni kavu tunapokwenda kulala usiku, na asubuhi tunapoamka tunaona kwamba ardhi imelowa maji, tutatambua kwamba mvua ilinyesha wakati tupo usingizini. Maji juu ya ardhi ni dalili ya kunyesha mvua.

Kwa njia ile ile, tunaweza kujua  kuhusu Mwenyezi Mungu kwa kutumia akili. Tunatazama katika ulimwengu na tunatambua kwamba ubunifu na mpango huu ulio kamili haungetokea bila ya kudura kuu, akili na uwezo wa kupanga na kuuamba. Lakini upo ulinganifu wa imani juu ya huu uitwao uhakika. Mtu mmoja huamini mvua kwa sababu ya mawingu ya mvua au maji juu ya ardhi, lakini yupo mtu mwingine ambaye aliiona mvua kwa kweli kwa macho yake. Mtu unaweza kusema kwamba, yapo maji juu ya ardhi lazima mvua ilinyesha usiku wa jana. Lakini atajibu, najua, nilikuwepo na niliona mvua mwenyewe. Mtu huyu ni shahidi wa mvua lakini mtu mwingine anaweza tu kutambua. Mwenyezi Mungu anasema kwenye Qur’ani:

“Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye elimu, wameshuhudia kuwa hakika hakuna aabudiwaye ila Yeye tu.” (Imran, 3:18)

Watu wengine wanaweza kutambua kuhusu Mwenyezi Mungu lakini wengine wanaweza kufikiriwa kama mashahidi kwa Upekee na Upweke Wake. Allamah Tabataba’i amesema kuhusu aya hii,

Wale wenye elimu hushuhudia kwamba hapana mungu ila Yeye. Hutazama na kutafakuri juu ya ishara Zake katika ulimwengu na ndani mwao wenyewe; na ishara hizo zimeshinda utambuzi wao na zimejikita kwenye kina kirefu katika akili zao.

Ishara hizi zimewasadikishia na wanaamini katika Upweke wa Mwenyezi Mungu kama mtu ambaye ameiona mvua na akaamini kwamba inanyesha. Baada ya kutambua vyema baraka za Mwenyezi Mungu, mtu anaweza kuwa na imani kama vile amemuona Yeye.

Qur’ani Tukufu inasema,

“Na ambao huyaamini uliyoteremshiwa wewe, na yaliyo teremshwa kabla yako, na Akhera wakaisadiki.” (al-Baqarah, 2:4)

Kwa hiyo tunaweza kuwa na uhakika kwa njia tatu. Njia ya kwanza ni kuwa na uthibitisho mkubwa mmo kwa kitu hivyo kwamba tunaamini kama vile tayari tumekiona kitu hicho. Njia ya pili ni kukiona kitu hicho sisi wenyewe kwa kweli. Na njia ya tatu ni kusikia na kukubali maneno ya mtu mwengine ambaye kamwe hangeweza kuongopa. Kwa hiyo wakati wowote Mwenyezi Mungu anapoahidi kitu upo uhakika kamili kwamba kile Alichosema ni kweli, na muumini asisite kutekeleza juu ya kitu hicho. Hii inajumuisha uhalisi wa maisha baada ya uhai wa hapa duniani na hayo mambo ya kiroho ambayo hatuwezi kuyashuhudia kimaumbile. Na pia inajumuisha manufaa ya Sharia ya Kimungu ambayo Mwenyezi Mungu ameanzisha. Hata kama hatujui sababu ya sharia au amri, tunatambua kwamba inayo manufaa makubwa kwa sababu inatoka kwa Mwenyezi Mungu, kama vile ambavyo hatuhoji manufaa ya baadhi ya dawa ambazo tunapewa na daktari mashuhuri.

2.              Nguzo ya Tatu - Uadilifu

Nguzo ya tatu ni Uadilifu. Kwa mujibu wa Uislamu, Uadilifu maana yake si sawa na ile ya jamii ya watu wa Magharibi. Katika jamii ya watu wa Magharibi Uadilifu kwa kawaida hulinganishwa na mojawapo ya vitu viwili. Kwanza hulinganishwa na kitu kilicho halali, hivyo kwamba kitu halali hufikiriwa kuwa haki na sahihi na kitu kisicho halali hufikiriwa kuwa dhuluma na kibaya. Pili, hulinganishwa na usawa, hivyo kwamba Uadilifu unaweza kufikiwa tu ambapo kila mtu anapewa sawa na kutendewa sawa na mtu mwengine, na dhuluma ni hapo ambapo mtu fulani anapata zaidi au anapungua au anatendewa tofauti na mwingine.

Lakini maana ya Uadilifu kwa mujibu wa Uislamu ni tofauti. Uadilifu maana yake ni kuweka kila kitu mahali kinapostahili kuwekwa kwa mpango unaostahili na kukipatia kila kitu kile kinachostahili. Maana yake ni kuweka katika mpango haki mtu alizonazo kwa Mwenyezi Mungu na haki alizo nazo mtu kwa muumbo wote. Maana yake ni kutekeleza yale yaliyo faradhi na kuepuka yale yaliyo haramishwa. Kile kilicho halali wakati mwingine kinaweza kuwa Uadilifu na wakati kinaweza kuwa ukandamizaji. Kutoa mimba, kunywa pombe, kusikiliza kile ambacho kimeharamishwa kusikilizwa na kutazama kile kilicho haramishwa kuona, kucheza kamari, uhusiano wa ngono wa watu wa jinsia moja, na maovu mengine mengi yote ni halali, lakini hiyo haina maana kwamba matendo hayo ni sahihi na adilifu. Na usawa wakati fulani unaweza kuwa adilifu na wakati mwingine ukandamizaji. Kuwalipa mshahara sawa wafanyakazi stadi na wasio stadi ni usawa lakini si uadilifu. Kuwapa wanafunzi wote darasani kiwango sawa cha kufaulu bila kujali utendaji wao ni usawa lakini si uadilifu. Kuwafanya mtu na samaki wote waishi kwenye maji ni usawa, lakini si uadilifu, kwa sababu binadamu atakufa. Kwa upande mwingine, kuwafanya samaki na binadamu waishi nje ya maji ni usawa lakini wala si uadilifu kwa sababu samaki atakufa. Mwenyezi Mungu anasema,

“Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na hisani na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu na uovu na uasi.” (An-Nahl, 16:90)

“Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamia uadilifu, mtoe ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu (juu ya) wazazi (wenu) na jamaa wa karibu.” (An-Nisa, 4:135)

“Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtoe ushahidi kwa uadilifu. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu. Fanyeni uadilifu, huko ndiko kunakomkurubisha mtu na ucha Mungu, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayo yatenda.” (Al-Maidah, 5:8)

Mtu mwenye imani anatakiwa kuwa muadilifu katika kila kipengele cha maisha yake kwa kiwango kwamba hapana yeyote atakayetarajia dhuluma ya aina yoyote kutoka kwake. Hata maadui na watu hao ambao mtu hawapendi, watarajie uadilifu kutoka kwake, kwa sababu muumini havuki mipaka iliyo wekwa na Mwenyezi Mungu.

3.              Nguzo ya Nne – Jitihada

Nguzo ya nne ni jihad, jitihada katika njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anasema:

“Wale walioamini na wakahama, na wakapigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, wana cheo kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na hao ndio watakaotengenekewa.

“Mola wao anawapa khabari njema za Rehema zitokazo Kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema zitakazodumu.”

“Watakaa humo milele, hakika Mwenyezi Mungu Kwake kuna malipo makubwa.” (At-Tawba 9:20-22)

Mtume wa Mwenyezi Mungu (S) alituma jeshi kwenye mapambano. Wapiganaji waliporudi aliwaambia, “Pongezi kwenu kundi lililotekeleza Jihad Ndogo, na Jihad Kubwa inawangoja.” Wakauliza “Jihad kubwa ni ipi?” Akajibu “Ni Vita ya kupigana na Nafsi.”

Maana yake ni kwamba, vita iliyo ngumu zaidi na muhimu zaidi ni mapambano ya kudhibiti matamanio yetu, na tusiyaruhusu yatudhibiti sisi.

Ni vigumu zaidi kudhibiti matamanio kuliko kupigana na adui, kwa sababu kupambana na matamanio haitegemei umbile. Hutegemea dhamira ya mtu. Binadamu anaweza kuwa na uwezo wa kunyanyua kilo 100 juu ya kichwa chake lakini hii haina maana kwamba anaweza kujidhibiti asitazame kitu kilicho haramu. Inapokuwa kitu ambacho Mwenyezi Mungu amekiharamisha inawezekana asiwe na uwezo kabisa. Kwa hiyo kwa jihad dhidi ya nafsi yake mwenyewe, hana silaha.

Mtu anayeomba lakini hafanyi juhudi ni sawa na yule anayetupa mshale bila shabaha. (Imam Ali (a.s.) katika Nahjul Balaghah semi Na. 337)

Kuomba kutoka kwa Mwenyezi haina maana kwamba tukae tuzembee bila kufanya kazi yoyote. Muumini anapofanya jitihada katika njia ya Mwenyezi Mungu na anaomba msaada, Mwenyezi Mungu atamwezesha kufuzu. Hii ni kwa sababu hakuna kitu kinacho patikana hapa duniani bila ya juhudi, na wakati mwingine watu hulalamika kwamba kufanya jema ni vigumu ambapo kufanya dhambi ni rahisi sana.

Tendo jema lina uzito zaidi mnamo Siku ya Hukumu kwa hiyo lazima lichumwe katika maisha haya. Ni rahisi kuchuma uovu hapa duniani lakini hauna faida yoyote kwako katika maisha yajayo.

4.              Nguzo ya Kwanza -  Uvumilivu

Miongoni mwa nguzo nne ya kwanza na muhimu zaidi ni uvumilivu, kama ambavyo Nahjul Balagha inavyosema.

Unatakiwa kutekeleza uvumilivu kwa sababu ustahamilivu ni kwa ajili ya imani kama vile kichwa kilivyo kwa mwili, hivyo kwamba kama ilivyo mwili usio na kichwa haukamiliki, imani isiyo na uvumilivu haikukamilika. (Nahjul Balagha, semi Na. 82)

Katika nguzo zote, uvumilivu ni muhimu zaidi kwa sababu huo ni uwanja wa majaribu ya imani ya mtu. Nguzo zingine zote tatu zinaweza kutekelezwa kama muumini anao uvumilivu. Mwenyezi Mungu anasema,

“Basi kwa hakika pamoja na dhiki iko faraja. Hakika pamoja na dhiki iko faraja.” (Inshirah, 94:5-6)

Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba kila baada ya tatizo patakuwepo na kipindi cha raha na starehe, na mtu anaweza labda kusema anaamini haya. Lakini tunawezaje kutambua kama anao uhakika? Kama akipatwa na tatizo na akastahamili kwa uvumilivu katika kipindi hicho kwa hiyo, utajua kwamba anao uhakika. Lakini kama hana uvumilivu na anafanya dhambi katika harakati za kutatua tatizo lake, kwa njia hiyo tutajua kwamba imani yake ilikuwa maneno tu hayakuwa matumaini ya kweli.

Uvumilivu ni wa lazima ili kuwa muadilifu, kwa sababu mtu lazima uvumilie majaribu ya kudanganya na kuiba vitu vya wengine. Endapo tupo katika hali mbaya kifedha tunatakiwa kuistahamili kwa uvumilivu hali hiyo na turidhike na chochote kile ambacho Mwenyezi Mungu anaturuzuku, tusipoteze utulivu wetu na kusahau haki za watu wengine. Inawezekana pawepo na fursa ya kuchukua njia mkato ili tupate fedha, lakini njia hizi za mkato humhusisha mtu kutokuwa mwaminifu na kuchukua rasilimali za watu wengine. Kama mtu anao uvumilivu, ataweza kutekeleza uadilifu katika shughuli zake zote za maisha yake.

Na bila shaka ni lazima kwa muumini kuwa mvumilivu kama anataka kujitahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Uvumilivu ni udhibiti na kujinyima ndio unao mlinda muumini asipotoke katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ni kama dereva ndani ya motokaa. Dereva anaweza akataka kwenda mwendo wa kasi lakini uvumilivu wake unahakikisha kwamba mguu wake haukanyagi sana kichapuzi. Dereva anaweza kutaka kubadilisha njia mara kwa mara na kwa hiyo kulazimika kuipita kila gari barabarani, lakini uvumilivu wake haumruhusu kukurupuka na usukani. Kama anabadilisha vijia, anaweza kuangalia kwa makini nani yupo karibu kwa kutazama tu kwenye vioo vyake, lakini uvumilivu wake utamwambia kufanya jitihada zaidi ya kugeuza kichwa chake ili awe na uhakika kwamba hakuna magari mengine yalioko karibu naye.

Kama mtu hana uvumilivu, itamwia vigumu sana kuwa na uhakika au kutekeleza uadilifu na kujitahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema, “Na tafuteni misaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa unyenyekevu.

“Na ombeni msaada kwa subira na swala na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu. Ambao wanajua kwamba wao ni wenye kukutana na Mola wao, na wao hakika ni wenye kurejea Kwake.” (Al-Baqarah, 2:45-46)

Mwenyezi Mungu anapendekeza kwako kwamba kama upo katika hali ngumu, kwamba wakati huu unatakiwa kutafuta msaada kwa uvumilivu na maombi. Maombi ni muhimu kwani hapana yeyote anayeweza kusaidia isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ni kutoka Kwake ambako tunatakiwa kuomba msaada. Na hadi hapo msaada huo utakapo kuja lazima tuwe wavumilivu, lakini kipengele hiki ni kigumu sana isipokuwa kwa waumini wa kweli. Katika hali yoyote tunayokabiliana nayo, uwezo wa kutenda uadilifu hutegemea kwanza kabisa ni sisi wenyewe kuwa na uwezo wa kujidhibiti. Kila tendo hutegemea uvumilivu wetu ili litekelezwe katika kipimo kinachostahili na hutulinda tusivuke mipaka. Nahjul Balagha inasema, ‘Uvumilivu ni wa aina mbili: uvumilivu juu ya matamanio kinachokupa maumivu, na uvumilivu dhidi ya matamanio.’ (Imam Ali (a.s.) Semi Na. 55)

Uvumilivu dhidi ya kile kinachotufanya tuhisi maumivu upo wazi. Maana yake ni kustahamili mabalaa na matatizo yanayo tupata katika maisha yetu. Uvumilivu dhidi ya kile tunacho kitamani maana yake ni uvumilivu dhidi ya kile ambacho matamanio yetu hututaka tufanye. Matamanio yetu hutuambia kwamba mali ya watu wengine inatakiwa kuwa yetu, kwamba anasa za dunia zinatakiwa kuwa zetu wakati wowote tunapozitaka, kwamba dhima na wajibu tulio nao hautakiwi kuwa wetu bali uwe wa watu wengine. Muumini lazima awe na uvumilivu dhidi ya majaribu haya kutoka kwenye nafsi yake, vinginevyo yatamwelekeza kwenye uovu.

Sifa za Sura Al-Hamd (Al-Fatihah)

Miongoni mwa Sura za Qur’ani Tukufu, Sura hii inayo hadhi ya juu, ambayo hunyanyuka kutoka kwenye sifa zifuatazo:

1.      Uzito wa Sura hii:

Kimsingi, sura hii inayo tofauti iliyo wazi na sura zingine za Qur’ani Tukufu kutokana na mtazamo wa uthabiti na uzito, kwa sababu sura zingine zote zinatoka kwenye usemi wa Mungu ambapo Sura  hii inatoka kwenye ulimi wa waja.  Na kutoka kwenye Mtazamo mwingine katika Sura hii, Mungu amewafundisha waja wake namna ya kusema na kuwasiliana na Yeye”

            Utangulizi wa Sura hii umeanza na kumsifu na kumtukuza Mola Mlezi.

            Inaendelea na imani  mwanzoni na baada ya maisha ya hapa duniani (kumtambua Mungu na imani katika ufufuo), inaisha na mahitaji na masharti ya waja.

           

            Wakati mtu mwenye hadhari, ambaye moyo wake umezinduka anasoma sura hii huhisi kwamba amewekwa kwenye mabawa na manyoya ya malaika, kwamba ananyanyuka kwenda mbinguni, na kwenye uwanja wa kiroho, hatua kwa hatua, anasogea karibu zaidi kwa Mungu (s.w.t.).

            Hili ni wazo bora sana, kwamba Uislamu, katika kukinzana na mifumo mingi ya imani za uwongo (ambapo husemekana kwamba wapatanishi wameteuliwa kati ya Mungu na muumbo,) umetangaza kwa wanadamu kwamba bila ya mpatanishi wanatakiwa kuanzisha uhusiano na Muumbaji wao!

            Sura hii ni mfano, ambamo uhusiano huu wa karibu kati ya Mungu na wanadamu imeegemezwa (bila ya wapatanishi), kati ya vilivyoumbwa na Muumbaji.  Mahali hapa yeye (mja) humuona Yeye tu, husema Naye tu, husikiliza ujumbe Wake kwa masikio yake na mwili wake, hivyo kwamba hapana hata Mtume au Mjumbe au mmoja wapo wa Malaika wa karibu sana anakuwa mpatanishi katika uhusiano huu.  Na inastaajabisha kwamba muunganiko huu na uhusiano wa moja kwa moja wa vilivyoumbwa kwa Muumbaji ni mwanzo wa Qur’ani Tukufu.

  • Sura Al-hamd, Msingi wa Qur’ani Tukufu.
  • Hadithi ya kutoka kwa Mtume Muadilifu (s.a.w.) tunasoma kwamba, “Al-Hamd ni Msingi wa Qur’ani Tukufu.” Na hii ilikuwa hapo ambapo Jaabir Bin Abdullah Ansari alikuja kumhudumia Mtume (s.a.w.), na Mtume (s.a.w.) alimwambia,

    ‘Ungependa nikufundishe sura iliyobora sana ambayo Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwenye Kitabu Chake?’ Jaabir alisema ‘Ndio, na iwezekane baba na mama yangu wajitolee muhanga kwako, nifundishe.’

    Hivyo Mtume (s.a.w.) alimfundisha yeye Al-Hamd, ambayo ni msingi wa Kitabu.  Na akaongeza kwamba Sura hii ni ponyo la kila maradhi isipokuwa kifo.’ (Majma’ul bayan, utangulizi wa Sura Al-Fatihah)

    Uthibitisho wa usemi huu unakuwa wazi kwa kutafakuri juu ya yale yaliyomo katika sura hii, kwa sababu kwa kweli, sura hii ni mkusanyiko wa yaliyomo kwenye Qur’ani Tukufu yote.  Mojawapo ya sehemu yake inahusu Upweke wa Mungu na kutambua Sifa Zake.  Sehemu nyingine inasema kuhusu yatakayotokea baada ya ufufuo na maisha ya baadaye.  Na sehemu nyingine inasema kuhusu mwongozo na kupotoka, ambao ni msitari wa tofauti, kati ya waumini na wasioamini.  Na pia, hapa inaonesha uwezo kamili wa Mola Mlezi, kituo cha Mamlaka, na ukarimu Wake usio na mwisho ambao hugawa kwenye pande mbili, upande wa ujumla na mahsusi (sehemu za Wingi wa Rehema na Usamehevu.)  Na hivyo hivyo inaonesha masuala ya ibada na utumwa, na kuwaelekeza wao kwenye Asili Yake iliyo takatifu.

    Kwa kweli, Sura hii ni mbainishaji wa Upweke wa Asili  (ya Mungu), Upweke wa Sifa (wa Mungu), Upweke wa ibada (kwa Mungu).

    Kutoka kwenye mtazamo mwingine, Sura hii inajumuisha viwango vitatu vya imani: kuamini kwa moyo, kushahidilia kwa ulimi na matendo kwa viungo.  Na tunatambua kwamba “Umm” inayo maana ya msingi na mzizi (kwenye fungu la maneno “Umm-ul-kitab” ikiwa na maana ya “Msingi wa Kitabu)

    Labda hii ndio sababu ambayo ibn Abbas, mfasiri mashuhuri wa Uislamu, anasema, “Upo Msingi kwa ajili ya kila kitu……….na msingi wa Qur’ani Tukufu ni Al-Fatihah.”

    Ni juu ya mwelekeo huu kwamba Mtume (s.a.w.) anasimulia kuhusu sifa za sura hii,

    “Kila Muislamu anaye soma Sura hii, thawabu zake ni sawa na yule ambaye amesoma theluthi mbili ya Qur’ani Tukufu (na kwenye simulizi zingine ni thawabu ya mtu ambaye amesoma Qur’ani Tukufu yote), na kama akikariri kwa ajili ya muumini yeyote mwanaume au mwanamke, atakuwa amempa zawadi.” (Majma-ul Bayan, utangulizi wa Sura al-Fatihah.)

    Kuhusu sura hii kuwa sawa na theluthi mbili ya Qur’ani Tukufu ni kwa sababu sehemu ya Qur’ani Tukufu inalenga kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), sehemu nyingine, inalenga kwenye Ufufuo na sehemu nyingine ni sharia na amri, na sehemu ya kwanza na ya pili zimo kwenye Sura Al-Hamdu.  Na uhusiano wake  (kuwa sawa na) Qur’ani Tukufu yote ni kwasababu, kutokana na mtazamo mmoja, Qur’ani Tukufu yote inaweza kufupishwa katika imani na matendo adilifu, yote haya yamekusanywa kwenye Sura Al-Hamd.

    3.      Sura Al-Hamd ni Fahari Kubwa  ya Mtume (s.a.w.)

    Ubora mkubwa ulioje kwamba kwenye aya za Qur’ani Tukufu Sura Al-Hamd imejulishwa kwa Mtume (s.a.w.) katika namna ya zawadi kubwa, na imeanzishwa sambamba na Qur’ani Tukufu yote, ambamo Anasema,

    “Na kwa hakika tumekupa (Aya) saba zisomwazo mara kwa mara na Qur’ani Tukufu (usemi huu unahusisha Sura Al-Hamd kuwa imeteremshwa mara mbili).” (Al-Hijr, 15:87)

    Qur’ani Tukufu pamoja na umashuhuri wake wote, katika mfano huu imewekwa sambamba na Sura Al-Hamd, na kuwa imeteremshwa mara mbili pia ni kwa sababu ya umuhimu wake mkubwa sana.

    Suala hili limetajwa kwenye simulizi kutoka kwa Mtume (s.a.w.) ambaye alisema, “Mwenyezi Mungu, Aliye Tukuka, amenipa upendeleo mahsusi kwa Wahyi wa Sura  Fatihah na Ameiweka sambamba na Qur’ani Tukufu Kuu, na Sura Al-fatihah ni miongoni mwa hazina zilizo thaminiwa sana kutoka kwenye hazina za Kiti cha Enzi (cha Mwenyezi Mungu).” (Tafsiri Burhan, Juz. 1, uk. 26)

    4. Msisitizo wa Kukaririwa Sura hii.

    Ikilengwa kwenye lugha ya ushawishi katika mazungumzo ambayo yanatupa mwanga kwenye sifa moja tu ya Sura Al-Hamd, inaonekana wazi kwamba kwa nini katika Hadithi za Kiislamu, kwenye makusanyo ya Shia na Sunni, msisitizo mkubwa umewekwa juu ya kukaririwa kwake.  Kukaririwa kwa Sura hii humpa mwanadamu zawadi ya kiroho na kiimani, humsogeza karibu zaidi na Mungu, huweka utakaso wa moyo na roho, huimarisha dhamira yake na huongeza haraka yake (ya kutembea) kwenye njia ya Mungu na muumbo. Na huweka kigingi kati yake na dhambi na kupotoka (kwenye njia iliyonyooka.)

    Kwa sababu hii, tunasoma kwenye simulizi kutoka kwa watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.).

          “Shetani aliomba na kulia kwa huzuni akiwa katika mateso mara nne.  Mara ya kwanza ilikuwa mnamo siku alipofukuzwa asionekane mbele ya Mwenyezi Mungu, halafu wakati alipoondoshwa kwenye Bustani na kupelekwa duniani. Mara ya tatu ilikuwa wakati wa kuanza kwa misheni ya Muhammad (s.a.w.) baada ya kutokuwepo kwa Mitume (a.s.), na kilio cha mwisho kilikuwa wakati Msingi wa Kitabu ulipoteremshwa.” (Noor-uth-Thaqalayn Juz ya 1, uk. 3)

    Yaliyomo kwenye Sura hii.

    Katika aya saba zilizomo kwenye Sura hii, kila moja wapo inaonesha jambo muhimu:

    KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

    Ni mwanzo wa kila kitendo, na inatupatia baraka kutoka kwenye Asili iliyo takasika  ya Mwenyezi Mungu kwenye kuanza kila kazi.

    SIFA NJEMA ZOTE NI ZA MWENYEZI MUNGU MOLA MLEZI WA VIUMBE VYOTE.

    Ni somo kutoka kwenye kupewa upendeleo wote, na maelezo kwa kila kiumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na inalengwa kwenye ukweli kwamba kila moja wapo ya zawadi hizi hububujika kutoka kwenye Asili yake iliyo Takasika.

    MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

    Amerudia jambo hili, kwamba asili ya muumbo, uelekezwaji wake na uwezo kamili juu yake vimekuwa kwenye nguzo za wingi wa Rehema na Urahimu.  Na msingi wa ubunifu na mpangilio wa ulimwengu huletwa na huu msingi (wa urahimu).

    MWENYE KUMILIKI SIKU YA MALIPO

    Hii inalenga kwenye maisha ya Akhera, kwa matokeo ya matendo na Uwezo kamili wa Mwenyezi Mungu juu ya sehemu hiyo kubwa ya ugawaji  (wa thawabu na adhabu)

    WEWE PEKEE TUNAKUABUDU, NA WEWE TU TUNAKUOMBA MSAADA.

    Hii inabainisha Upweke katika kuabudiwa na Upweke katika jambo la tegemeo la mwanadamu.

    TUONGOZE KWENYE NJIA ILIYO NYOOKA.

    Hii ni bainishi ya uhitaji na upendo wa waja kwa suala la mwongozo, na pia inalenga kwenye ukweli kwamba miongozo ya amri zote inatoka Kwake!

    Baada ya kutazama aya ya mwisho ya Sura hii, ni dhahiri na wazi kutoka………..(njia iliyo nyooka) kwamba ni njia ya watu hao ambao wameingizwa kwenye baraka Zake.  Na wametengwa kutoka kwenye njia ya hao  ambao wamepokea ghadhabu na hao ambao wamepotoka.

    Kutoka kwenye mtazamo mmoja sura hii imegawanywa katika sehemu mbili, upande mmoja ni ule unaosema juu ya sifa na kutukuzwa kwa Mwenyezi Mungu na sehemu nyingine juu ya mahitaji ya waja.

    (Hii ni) sawa tu kama kwenye “Uyoon-ul-Akhbar” kwenye simulizi kutoka kwa Mtume (s.a.w.) tunasoma,

    “Mwenyezi Mungu Aliye Tukuka amesema, ‘Nimeigawa Sura Al-Fatihah kati Yangu Mwenyewe na mja Wangu, nusu yake ni kwa ajili Yangu, na nusu nyingine kwa ajili ya mja Wangu, na mja Wangu anayo haki kwamba chochote anachotaka anatakiwa aombe kutoka Kwangu.’

    Mja anaposema, ‘Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu,’ Mwenyezi Mungu Mkubwa husema, Mja wangu ameanza kwa jina Langu, na ni juu Yangu kuchukua kazi zake na kuzimalizia, na katika kila hali ajaziwe baraka.’

    Na mja anaposema, ‘Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa Viumbe Vyote.’ Mwenyezi Mungu Mwenye kutukuka anasema, mja wangu ameanza kwa jina Langu, na anajua kwamba baraka alizo nazo zinatoka Kwangu, na pia Nimeondoa mateso yake na kuwa mbali nayo, muwe mashahidi (Enyi Malaika) kwamba nitazifanya baraka zake za akhera kuwa kubwa zaidi kuliko baraka zake za duniani na nitayafukuza majanga ya ulimwengu huu kutoka kwake, kama vile Nilivyo yaondosha majanga ya ulimwengu huu.’

    Na mja anaposema, ‘Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu’, Mwenyezi Mungu anasema mja wangu ameshahidilia kwamba, Mimi ni Mwingi wa Rehema na Mwenye Kurehemu, hivyo kuweni mashahidi  kwamba nitamfanya abubujikiwe na rehema Zangu, na na mimi nitafanya sehemu yake kutoka kwenye Urehemevu Wangu daima milele.’

    Na mja anaposema, ‘Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo,’ Yeye husema ‘Muwe mashahidi kwamba anapokiri kwamba Utawala na Umiliki wa Siku ya Malipo ni Wangu, mnamo Siku ya Hesabu, Nitafanya hesabu yake kuwa rahisi, Nitakubali matendo yake yaliyo adilifu na nitasamehe dhambi zake.’

    Na mja anaposema, ‘Wewe Pekee tunakuabudu,’ Mwenyezi Mungu Aliye Tukuka husema, ‘Mja Wangu husema kweli, huniabudu Mimi tu, Nitakufanyeni, mashahidi kwa ibada hii ya uaminifu, Nitampa thawabu ambayo kwamba yeyote ambaye alikuwa dhidi yake atastaajabu kwa hali atakayo kuwa nayo.’

    Na mja anaposema, ‘Na Wewe Tu Tunakuomba Msaada,’ Mwenyezi Mungu husema, Mja Wangu ameniita Mimi, na ametegemea Kwangu tu, kuweni mashahidi kwamba nitamsaidia yeye kwenye shughuli zake, kwenye matatizo Nitakuwa naye kwa ajili yake, na katika siku ya huzuni Nitamshika mkono wake.’

    Na mja anaposema, ‘Tuongoze Kwenye Njia Iliyo Nyooka………’ (hadi mwisho wa Sura), Mwenyezi Mungu husema, Ombi hili la mja Wangu limekubaliwa, na chochote anachotaka anatakiwa kuomba kutoka Kwangu kwani Mimi nitakubali chochote anachotumaini na kumpa, na wakati wowote anapotaka usalama Nitamsalimisha. (Uyoon Akhbar cha Imam Reza  (a.s.)).

    KWA NINI JINA LA SURA HII NI FATIHATUL-KITAB?

    Fatihatul-Kitabu inayo maana ya “mwanzo” (au utangulizi, dibaji, na kadhalika), na kutoka kwenye simulizi tofauti ambazo zimesimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.), inaweza kueleweka vema sana, kwamba Sura hii ilijulikana kwa jina hili wakati wa kipindi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.).

    Ijapokuwa Sura Al-Hamd haikuwa Sura ya kwanza kuteremshwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.), Qur’ani Tukufu ilipangwa wakati wa kipindi chake Mtukufu Mtume (s.a.w.) kama hivi ilivyo sasa, na mwanzo wake ulikuwa ni Sura hii hii ya Al-Hamd.

    Nyaraka nyingine nyingi zipo ambazo zina thibitisha ukweli huu, kwamba Qur’ani Tukufu katika umbo ilivyo leo, ilipangwa kwa amri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w)

    Uthibitisho mwingine ni kwamba Khwarizmi, mwanachuoni maarufu wa Madhehebu ya Ahlu Sunna, kwenye kitabu kiitwacho “Manaqib” anasimulia kutoka kwa Ali ibn Riyah ambaye anasimulia kwamba Ali Bin Abi Talib na Abi ibn Ka’b walikusanya na kuipanga Qur’ani Tukufu wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

    Ushahidi wa tatu ni usemi kwamba Hakim, mwandishi mashuhuri ameleta kutoka kwa Zayd Bin Thabit, kwenye kitabu chake “Mustadrak” kwamba Zayd anasema.

    Sisi, tuliokuwa kwenye huduma ya Mtukufu Mtume (s.a.w.), tulikuwa tunaikusanya Qur’ani Tukufu kutoka kwenye sehemu zilizo sambaa, na kila mtu, chini ya uongozi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.), aliiweka mahali pake mwenyewe panapo stahiki.  Lakini kwa njia hii maandishi bado yalikuwa yamesambaa, hivyo Mtukufu Mtume (s.a.w.) alimuelekeza Ali (a.s.) kuikusanya (na kuipanga) Qur’ani Tukufu, na alituonya isije ikapotea.”  “Qur’ani Tukufu wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.) ilipangwa na kuwa katika umbo hili ilivyo sasa.”

    Kwa hali yoyote, kwa dhati, hadithi mashuhuri ya “Thaqalayn” kwamba umma wote wa Waislamu wanakubaliana pale Mtukufu Mtume (s) aliposema, “mimi ninaondoka miongoni mwenu na ninawaachieni vitu viwili …….” Kimojawapo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) inaonesha kwamba Qur’ani Tukufu tayari ilikwisha kusanywa kuwa kitabu kimoja kilicho kamili.

    Na kama tumeona simulizi ambazo zinatoa uthibitisho wa kukusanywa kwa Qur’ani Tukufu na kundi la masahaba chini ya usimamizi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.), zinasimulia idadi tofauti za watu na haileti tatizo lolote; inawezekana kwamba kila simulizi inataja baadhi yao tu.

    Majina yake

    Wametaja majina mengi; yaliyo maarufu ni haya yafautayo:-

    1 – Faatiha (ufunguzi): Kwa sababu ndiyo sura ya kwanza katika msahafu, na ni wajibu kuisoma mwanzo wa swala.

    2 – Al-Hamdu: kwa sababu ndilo tamko la mwanzo katika sura hiyo.

    3 – Ummul-Kitab na Ummul-Qur’an (mama wa Qur’an): kwa sababu imetangulia sura nyingine, ijapokuwa ni kwa kimandishi tu.  Kwani mama huwatangulia wanawe.  Na kwa vile imekusanya misingi miwili; kutaja utawala wa Mungu na utumwa wa mja, na mambo mawili hayo ndiyo nguzo ya mafundisho ya Qur’an.

    4 – Sab’ul Mathani (Saba mbili) kwa sababu ina aya saba, au ina Aya saba zinazorudiwa mara mbili katika swala, au ni kwa sababu inataja mambo mawili:  Mola na mja wake.