Uliniandikia kua “ hivi ni kwa nini mwanamke akitaka
kusali ni lazima avae hijabu hata kama atakua yupo peke yake ndani ya nyumba”?
Dada yangu daima usisahau ya kua Mola wako siku zote
huwatakia waja wake kheri na maslahi, na hakuna hata sheria moja ya Mola wako
isiyokua na hekima, ima waja waifahamu hekima hiyo au wasiifahamu, hii ni
sheria ya Mwenyezi Mungu, vile vile ndani ya sheria hii mna hekima, na miongoni
hekima hizo ni hizi zifuatazo:-
1. Mazowezi ya kumpandisha mtu daraja.
Sala ina fadhila nyingi, na vile vile ni moja
kati ya mazowezi ya kumpandisha mtu daraja, ndani ya sala sisi tuna mambo
chungu nzima tunayojizoweza nayo, kama vile kumpwekesha Mola, kumkhofu, pamoja
na kusoma Qur’ani, basi sala kitu kimoja kilichokusanya mambo tofauti yenye
thamani, na hijabu kwa wanawake ndio hivyo hivyo, kama vile Mola asemavyo na
Qur-ani inavyosema, hijabu kwa mwanamke huwa inampa thamani maalum mwanamke, na
ni moja kati ya mambo yenayomkamilisha mwanamke huyo.
2. Kutangaza rasmi kumtii na kumcha Mwenyeezi Mungu
Mkuu wa jeshi anawaambia wafuasi wake, “mwanajeshi
mzuri na mwenye kujua wadhifa ni lazima siku zote afike uwanjani hali ya kuwa
amevaa fomu.
Sasa fikiria iwapo mwanajeshi mmoja atataka kuonana na
mkuu wa jeshi wakati anapokwenda Idarani kwake, ikisha yeye avae fomu
anapokwenda kuonana nae, kufanya kwake hivyo kutakuwa kutamaanisha kwamba yeye
amekubali kufuata amri ya mkubwa wake.
Kwa hiyo basi, kuhudhuria pahali alipokuwepo mkubwa
wako huku ukiwa katika utaratibu kamili alioutaka yeye, kutakuwa kunaelezea
utiifu wa mtu huyo hata kama hakuzungumza kwa ulimi wake.
Mwanamke muislamu ambaye ameahidiana na Mola wake
iwapo atakwenda mbele ya Mola wake na hijabu, kwa ajili ya kutekeleza amri ya
Mola wake basi atakuwa yeye anamtangazia Mola kuwa yeye yuko tayari kufuata
amri zake na ameridhika na Mola wake.
WASIA
WA MWISHO
Dada yangu we mimi nakutaka uyatie akilini
na uyafikirie yale yote niliyokuandikia, na jaribu kufikiria zaidi kwamba dunia
ni yenye kupita, ujana nao unakimbia kwa nguvu, kuna wangapi waliokuwa wana
ndoto za uzuri na walikuwa wakishindana katika kuolewa na leo wako chini ya
udongo, na nyuso zao zilizokuwa nzuri pamoja na miili yao haikubakia isipokuwa
mifupa tu, kilichobakia ni amali zao tu, iwapo walitenda amali.
Kila mtu katika shule hii ya dunia ana
faili lake, na akimaliza shule faili lake bado litabakia, dunia ni soko wako
wenye kufaidika katika soko hilo na wako wenye kula hasara, siku zote katika
soko hili hutoka watu na kuingia wafanya biashara wengine, basi kama vile
unapokuwa muangalifu unapochagua kitambaa unapokuwa dukani, basi amali na
matendo yako kuwa muangalifu nayo, na mwishowe niliyokuandikia katika barua hii
yachunguze na uyalinganishe, na Mola wako atakuongoza katika njia iliyo sawa. |