Salamu alaikum dada mpendwa.
Barua yako ambayo umeniandikia nimeisoma.
Mimi suala la kuvaa hijabu kwa kumuiga mama yangu tu na bila ya kujua umuhimu wake silikubali, kwani sitaki niwe ni miongoni mwa wenye kuabudu mila zisizokua na msingi, sitaki kutolewa thamani, wala kua niko nyuma bali nataka niwe kama walivyo watu wengine katika jamii, mimi sitaki kutekeleza matakwa ya wazee bila ya kujua malengo yake, kwanza hasa nataka muniambie ni wapi Qur’ani imemtaka mwanamke avae hijabu? La pili ni kwa nini wanaume wawe huru na wawe wanatenda walitakalo, lakini wanawake wawe wamewekewa mipaka na vikwazo, na kwa nini hamutaki watu kuwawacha huru na kuyawachia mambo yaelekee kwa mtiririko wake wenyewe, kwani mkifanya hivyo mtaisalimisha jamii kutokana na msuguano, nyinyi mmeifanya dini kua nzito na mambo mkayafanya magumu, mpaka mmefikia kumtaka mwanamke hata kama atakua yupo peke yake na akataka kusali basi ni lazima avae hijabu, hivi nyinyi mmemfanya Mungu kua ni mwanamme kiasi ya kwamba sisi tujistiri mbele yake? Nataka kujua hasa kutokuvaa kwangu hijabu kunamdhuru nani katika jamii? Mimi najipamba nitakavyo na ninavaa nguo nitakazo, mambo yangu mimi yanakuhusuni nini? Mimi sifanyi hivyo kwa ajili ya kuleta ufisadi, halafu ni kwa nini hamuwaambii wanaume wasiwaangalie wanawake bali mnatuambia sisi tuvae hijabu? Samahani msije mkanifikiria mimi kua sina dini au ni kafiri, amini usiamini mimi ni kama wewe namkubali Mwenyeezi Mungu na vile vile naikubali Qur’ani nami ni muumini wa kweli, na wala sitaki kukosa radhi za Mwenyeenzi Mungu, mimi sio miongoni mwa wale wasiojua fadhila, naelewa kuwa Mwenyeenzi Mungu amenipa neema chungu nzima, mimi niko katika bahari ya neema zake, na napenda kila siku nizidi kuwa karibu nae, na nimridhishe zaidi, na niwe muangalifu zaidi katika masuala tofauti, na niyaelewe undani wake masuala hayo, ili niishi katika njia iliyo sawa, na siyo niishi kama vile wanavyotaka watu, mimi nasema kwamba iwapo kuna watu chungu nzima wasiokuwa na hijabu basi kuvaa hijabu kwangu mimi kutakuwa na faida gani? Itakapokuwa kutokuvaa hijabu kwangu mimi kutasababisha watu kupotea basi tujaalie kwamba mimi nitavaa hijabu lakini kuna watu wangapi wasiovaa hijabu? Ambao bado watakuwa ni kizuizi na watakuwa ni sababu ya kuwapoteza watu, basi kuvaa au kutokuvaa hijabu kwangu mimi kuna tofauti gani? Ukiachia yote hayo lakini hebu nambieni hivi nyinyi ni kwa nini mnayafanya mambo kuwa ni magumu, na hata nywele moja ya mwanamke hamutaki ionekane, mimi nataka kuelewa nywele moja ina tatizo gani kuonekana, na italeta madhara gani, wewe ni lazima unipe mimi haki katika suala hili, na baadae nataka unieleze ni kitu gani kitakachonifanya mimi niwe na hijabu, na vipi mimi nitaweza kulikubali suala hili.
Kwa kweli barua yako nimeipata na imenifikia, na kusema kweli mwanzo nilikuwa sina shauku ya kukuandikia jawabu kuhusu masuala yako, lakini baadhi ya ibara zako zimenilazimisha mimi kukamata kalamu na kukujibu, ingawaje ni kwa ufupi kabisa, na ibara zenyewe zilizonisababisha
Kujibu ni hizi zifuatazo:
Mimi sitaki kufanya jambo nisilolijuwa malengo yake.
Mimi naikubali Kur-ani.
Mimi napenda Mwenyeenzi Mungu awe radhi nami.
Baada ya kuziona ibara hizi nikasema mwenyewe kwa mwenyewe:
Nitamuandikia ukweli ulivyo, itakapokuwa ni kweli anataka kuelewa ukweli ulivyo na iwapo ni kweli wewe unatafuta radhi za Mwenyeenzi Mungu basi utatoa muda wako kwa ajili ya kuyafikiria mambo haya, na utaitupia macho kur-ani, na pale utapoona.
kwamba maneno yangu yana ushahidi wa Kur-ani na yanakubaliana na akili basi utayakubali, na iwapo wewe utakuwa huko katika kutafuta ridhaa za Mwenyeenzi Mungu na wala hutaki kuujuwa ukweli, na kwa kweli samahani sivyo kama vile mimi nnavyofikiria hivi kwa nini usiwe ni mwenye kutafuta radhi za Mwenyeezi Mungu, na ni kwa nini usitake kuujuwa ukweli? Kwani hii dunia na vilivyomo ndani yake vina thamani gani? Vitakavyomsababisha mtu aridhike na maisha haya mafupi ya dunia, na kutupilia mbali mambo ya kiakili na ya imani, na kuyafumbia macho mambo hayo, mimi nnaelewa kwamba wewe unataka kufahamu, na unataka kuishi katika jamii kwa kupitia ufahamu wako na kuelewa kwako,na kwa sababu mimi nimefahamu hilo ndio maana nikaamuwa kuijibu barua yako. Ili jawabu yako iwe wazi zaidi nimeamuwa maneno yako kuyafupisha katika vipengele kumi, na nnakuandikia kwa ajili yako, kisha naanza kujibu kipengele kimoja kimoja, nafanya hivyo kwa kutegemea kuwa maelezo yangu utayasoma kwa uangalifu, na utakaa katikati bila ya kutilia uzito upande Fulani, na nakutaka uyaangalie kwa makini, na lile utakaloliona ni sawa basi likubali:
1. Kutokuwa na hijabu kwa wanawake kuna madhara gani kwa watu wengine.
2. Hivi katika Qur-ani suala la ulazima wa kuvaa hijabu kwa wanawake limezungumzwa
3. Kuna msukumo gani unaoweza kulifanya suala la hijabu kuwa ni la lazima na kwa lugha nyengine, nini hasa falsafa ya kuvaa hijabu?
4. Kwa nini hamuwaambii wanaume wasiwaangalie wanawake, ili wanawake waepukane na shari ya kujifunika maguo.
5. Ni kwa nini wanaume wamepewa ruhusa ya kufanya walitakalo na wavae watakavyo, lakini wanawake wakawekewa vazi maalum
6.Ni sawa kabisa mimi silitilii maana suala la kuvaa hijabu, na nnavaa nguo nzuri na kujipamba kisha nnatoka mbele za watu, lakini sina makusudio ya kusambaza upotofu na ufisadi.
7.Kwa kupatikana watu wengi wasiokuwa na hijabu kwa hali yoyote ile ufisadi utapatikana, basi kuvaa au kutokuvaa kwangu mimi hijabu kutakuwa na tofauti gani?
8.Itakapokuwa wanawake wote wana uhuru wao basi suala hili litakuwa ni la kawaida katika jamii.
9.Kwa nini hata nywele moja ya mwanamke haitakiwi kuonekana, huu unywele mmoja wa mwanamke una madhara gani kuonekana.
10. Hivi ni kwa nini mwanamke atakapokuwa peke yake ndani ya nyumba na akawa anasali ndani
Anatakiwa kuvaa hijabu?
JAWABU:
1. Kutokuvaa hijabu wanawake kuna madhara gani kwa wengine?
Katika kujibu suala hili kwanza naanza kukusimulia maneno ya mwana biashara mmoja, yeye anasema hivi uislamu unataka aina ya ladha za kijinsia uzitenge kwenye masuala ya ndoa tu, ladha hizo ziwe za aina yoyote ile, za kuangalia kwa macho au za kugusana kimwili, na masuala ya ndani ya jamii yawe yana uhusiano na mambo ya kikazi za kijamii, tofauti na mfumo au mtizamo uliokuwa sio wa kiislamu ambao kazi za kijamii na masuala ya kijinsia yanaendana pamoja, kwa hiyo uislamu unataka kutofautisha masuala mawili haya.
Kwa maoni yako ikiwa sehemu za kufanyia kazi, sehemu za kutafuta elimu, kufanya tahakiki, kuzalisha au kukuza vitego tofauti vya kiuchumi ikiwa zitakuwa zimeepukana na wasiwasi wa masuala ya kishetani na mambo ya uchafu maendeleo yatakuwa ni mengi na bora zaidi au ikiwa sehemu hizo zimezungukwa na masuala machafu ya kijinsia yanaweza yakapatikana maendeleo bora?
Kutokuwa na hijabu kwa wanawake na kuwepo mchanganyiko baina ya wanawake na wanaume katika sehemu za kazi ndiko kunakosababisha madhara na uharibikaji wa jamii, ambapo ikiwa watu watayazingatia masuala haya basi kutaipelekea jamii kuishi kwa amani bila ya ufisadi na wala hakuna mtu yoyote sio mwanamke wala mwanamme ambae hatoridhika na hali hiyo.
Dada mpendwa mimi nna uhakika kwamba ikiwa utazingatia haya nnayokuandikia, na ukafahamu kwamba kuna madhara gani yanaweza kutokea kwa watu na jamii kwa ujmla ikiwa masuala ya kutokuvaa hijabu hayatatekelezwa, na wewe mwenyewe hutokuwa tayari kushuhudia madhara hayo.
Mimi nakuandikia kwa ufupi tu madhara ambayo yanaweza kutokea katika jamii ikiwa masuala ya kuvaa hijabu hayatozingatiwa.
Itakapokuwa wanawake na wanaume wanachanganyika pamoja itapelekea matamanio ya nafsi kwa watu na jamii, na kama inavyoeleweka kwamba nafsi ya mwanaadamu haitosheki,na kila siku zinapokwenda inazidi kuongozeka kama moto ambao unachocholewa kwa kuni, na mwanaadamu akishafikia katika hali hii ni tabu sana kujirekebisha, katika hali hii basi utamkuta mwanaadamu amepoteza mahitajio yake, matokeo yake anakuwa ni mwenye tabia mbaya za kishetani, asie jiamini, na mwenye wasi wasi.
Mwanamme ambae kila siku atakuwa anaonana na wanawake ambao wamejipamba na wasiovaa hijabu, na akawa anakabiliana nao katika pirika zake za kikazi za kila siku, akawa anaona uzungumzaji wao, tabasamu zao, na wakati anaporudi nyumbani akamkuta mke wake katika hali isiyokuwa nadhifu, amechoka na kazi za nyumbani za mchana kutwa hatokuwa na shauku hata hata ya kumuangalia mke wake, katika hali hii basi mwanamme huyo atakuwa na nguvu za kumlinganisha mke wake na wanawake ambao amewaona nje, matokeo yake atadhania kwamba haiwezekani kuishi na mke wake na mwisho wa mambo utakuta anamuacha mke wake, na mara nyingi utakuwa umeshashuhudia au umeshasikia kwamba mwanamme fulani ameoana na mfanyakazi mwenziwe, na mke wake wa mwanzo amempa talaka.
Kuongezeka kiwango kikubwa cha talaka ni kuongezeka kwa watoto wakimbizi, na watanga na njia wasiokuwa na kazi, na kama utazingatia mara nyingi watoto kama hao ni tofauti iliyotokea baina ya wazazi wao, na kutokupendana na kutosikilizana baina ya mke na mume katika kuendeleza maisha yao.
Dada mpendwa kwa maoni yako wewe unafikiri ni kwa nini vijana wa zama hizi hawapendi kufunga ndoa? Katika zama za zamani wanawake walikuwa ni wenye heshima na wenye kuhifadhika zaidi kuliko zama za sasa hivi, kila kijana alikuwa akipendelea kufunga ndoa, na walikuwa wakiowa wakiwa na miaka kidogo tu (yaani baada ya kubaleghe), ama bahati mbaya katika zama zetu hizi za sasa hivi tunaona kwamba vijana wengi wanapopendelea kukidhi mahitajio yao ya kibinafsi huenda kutafuta watoto wa watu, au hutafuta wanawake ambao masuala ya hijabu kwao wao sio muhimu, na wanapofunga ndoa ni kwa sababu tu wamelazimishwa na wazee wao, na wanakuwa hawana furaha katika maisha yao.
Hivi ni kweli kama ingelikuwa vijana hawawaoni wanawake katika hali ya kujipamba na kutembea bila ya hijabu hali ingelikuwa ni hii hii? La ! sifikirii,
Ni mtu gani anaekubali kuona familia yake, au watoto wake wako katika hali hii ya maisha?
Hivi mwanamke ambaye haoni umuhimu wa kuvaa hijabu, na anajipamba na kutembea barabarani, au sehemu za kazi hivyo anaelewa kwamba anakiuka sheria za Mwenyeenzi Mungu? Au inawezekana anafanya hivyo kwa kukusudia.
Dada mpendwa mimi nakuuliza suala:
Katika sehemu za kazi ambazo ni wanawake watupu au wanaume watupu, kazi zinakuwa zinafanywa kwa mazingatio zaidi au katika sehemu ambazo kila siku na kila wakati wanaume wanakabiliana na wanawake katika hali ya mapambo na kutokuwa na hijabu?
Hivi katika skuli au katika vitengo vya kujipatia elimu ikiwa wanafunzi wanawake na wanaume wako pamoja na wana maelewano katika masuala tofauti ikiwa ya kijinsia au hata namna ya kuvaa kwao kwa nguo, kutembea kwao, mazungumzo yao n,k…….katika hali hii wana nafasi ya kushughulikia masomo yao, au ikiwa skuli za wanafunzi wa kike na wakiume mbalimbali?
Ni jambo lililowazi kwamba mchanganyiko wa wanawake na wanaume, na kutozingatia masuala ya kujistiri au kuvaa hijabu ndiyo inayosababisha kuharibika kwa mioyo au akili za baadhi ya wanawake na wanaume, na kupelekea kutokufanya kazi vizuri, mbali ya haya inatokea wakati unamkuta kijana anapenda kufanya kazi na kukuza uchumi, lakini anapokumbana na ufisadi katika jamii yaani anapokuwa na uhusiano na wanawake ambao hawajistiri au hawavai hijabu utamkuta mtu huyo hana shauku ya kufanya tena kazi na anakuwa wakati wote yuko katika fikra potofu za kujenga uhusiano na wanawake hao, matokeo yake kijana huyo anaishia jela au anakuwa ni mvuta bangi, basi kutokea kwa matatizo haya ingelikuwa kijana huyo alisema na nafsi yake na akawa hayuko tayari kujishughulisha na ufisadi huo angelikutwa na matatizo hayo?
Wezi siku zote wanaendelea kuiba na kufosi mali za wengine, ama mtu atakapokuwa yeye mwenyewe hatafanya hadhari na akauwacha wazi mlango wa gari yake au mlango wa nyumba yake, au dhahabu na fedha zake, akawa hakuzihifadhi, basi mtu huyo atakuwa yeye mwenyewe amewatangazia wezi ghanima, kwa sababu kufanya kwake hivyo kunawarahisishia wezi kazi. Basi mambo ndio hivyo hivyo kwa upande wa watu wenye maradhi ya moyo, na wenye kuabudu matamanio yao, wanapomuona mwanamke aliekuwa hajajihifadhi au amejipamba hali akiwa ndani ya jamii ya watu mambo hayo yanawachochea zaidi na kuwasindikiza katika ufisadi, hapo basi huanza kumfuata fuata mwanamke huyo na kumuudhi, na inaweza kupelekea mwanamke huyo kuvunjiwa heshima yake au hata kupoteza roho yake, kuna wanawake wangapi hadi leo walioingia katika mikono ya mafisadi na kupata matatizo mbali mbali, iwapo wewe utakuwa umehudhuria mahakamani au umeyakagua mafaili ya vikundi vya kihuni yaliyoko mahakamani, utakutia kwamba waliotiwa mikononi na vikundi hivyo miongoni mwa wanawake wamepata mateso kutoka katika vikundi hivyo na hadi kupoteza roho zao,na wanawake hao waliopata matatizo hayo walikuwa ndani ya jamii hawajihifadhi kwa kuvaa nguo za heshima, na kwa bahati mbaya matokeo kama haya ya hatari yamezidi kuwa mengi katika jamii, na nna uhakika kabisa kwamba wanawake hao waliopata matatizo walikuwa hawana malengo ya kuvuruga amani katika jamii, na wala walikuwa hawajachoshwa na maisha ya duniani, lakini wao walikuwa wakipendelea tu kuonekana katika jamii huku wakiwa wanatembea barabarani, na hali wakiwa wamevaa nguo wazipendazo, huku wakiwa wao wameghafilika na matokeo yatakayotokea baadae, basi kudumu kwa vitendo kama hivyo kunasababisha kutopatikana amani ya mtu binafsi na katika jamii.
kuwa na uhusiano nao, basi hapo nafasi asili ya mwanamke, na sifa maalum alizokuwa nazo zitakuwa ni zenye kusahaulika na badala yake mwanamke atakua ni kama chombo cha kujistareheshea au kuchezewa na wanaume tofauti, na katika taratibu kama hizi mwanamme atakuwa hamthamini mkewe, na atasahau ladha ya chumvi, kwa sababu kiwango chochote kile cha wanawake akitakacho atakipata kwa sababu wako wengi wamemwagwa barabarani, ni maana mbaya ilioje iliyobeba sentensi hii, na ni makosa mazito yalioje kwa wale wenye kusababisha thamani ya mwanamke ishuke hadi kufikia kiwango hichi, na chenye kuumiza zaidi ni kule kupata nafasi watu wenye kuabudu pesa na wenye kuabudu dunia katika kuwaharibu wanawake na kuwafanya wao ni bidhaa, bali bidhaa ina thamani zaidi.
Ni jambo la kusikitisha mno kuona kwamba kwa ajili ya kutafuta soko la magazeti, na kwa ajili ya kutafuta pesa, utakuta juu ya gazeti huchapishwa picha ya mwanamke, au kwa ajili ya kuwavuta wateja utakuta mtu anamuweka mwanamke dukani, na kwa ajili ya kuwavutia watizamaji watu hutafuta film za wanawake wenye kujionesha, jee! Kufanya hivyo si moja kati ya njia za kumvunjia mwanamke heshima, na kuitoa thamani nafasi ya mwanamke? Na jee wanawake ambao hawajihifadhi na macho ya wengine hivi hawasababishi kuvunjiwa heshima wao wenyewe pamoja na wanawake wengine?
Suala la wanawake kuwafanya ni chombo na kutumia vibaya uzuri wa nyuso zao limeenea kiasi ya kwamba baadhi ya wakati utakuta katika gazeti kuna nyuso za wanawake ambao ukiwaangalia utaelewa kwamba wana ujuzi Fulani, na wanatoa ujumbe fulani, na wenyewe wanaamini ubaya huo, wanakiri suala hilo, basi angalia maneno haya ya mchezaji wa snema maarufu anavyokiri:
“mimi mwenyewe ni nyota nikimaanisha kwamba sio mtu ambae nnadhamini na kuzifanya film zinunuliwe, watowaji makosa na wasambazaji magazeti katika masuala ya film zangu wao hawaangalii sana namna ya uchezaji wangu wa snema, bali wanaangalia kitu chengine, katika zama hizi mimi nnajihisi vibaya sana, na kitu kibaya kabisa ni kwamba mchezaji wa film hufikia wakati yeye mwenyewe akajua kwamba watizamaji wanakuja kuangalia sinema kwa ajili ya uso wake wenye kupendeza, na wala sio kwa ajili ya namna ya uchezaji wake wa film, mimi mwenyewe nimeufikia uhakika huu mchungu, na nimeamua kufikiria upya kabisa kuhusu na uchezaji wangu wa film.
Ni sawa matokeo haya ni mabaya yalioje kwamba badala ya mtu kuangalia sanaa na uzuri wake au kutupia jicho elimu pamoja na kuangalia juhudi, juhudi ambazo zinampelekea mtu kuongeza ujuzi wake, basi jamii hutupia macho na kuangalia nyuso na matamanio yao.
Ama ni lazima tupate jawabu la suala hili lisemalo ni mtu gani ikiwa wanawake watazingatia masuala ya kuvaa hijabu na kujistiri, na wasikubali kuwa ni kama chombo cha kustareheshea kinachotumiwa na wanaume, basi ufisadi huu ambao sasa umeenea katika jamii utatoweka.
Sasa hivi nnaifafanua nukta ya pili ambayo uliielezea.